Jinsi ya Kupika Mtori Mtamu Sana - Pishi la Kichaga



Mtori ni chakula maarufu sana kwa watu wa kaskazini huko hasa hasa mkoa wa Kilimanjaro. Na kwa sasa maeneo ya mjini mtori umekuwa unanywewa sana mida ya asubuhi kama kifungua kinywa. Sasa leo nakuelezea namna ya kupika mtori mzuri na mtamu.

Mtori kwa watu 3

MAHITAJI


  • Ndizi bukoba 10 
  • Nyama ya Ng'ombe 1/2 kg ( hapa waweza tumia hata nyama ya kuku, nguruwe, mbuzi nk)
  • Vitunguu maji 2 ( vimenywe na kukatwa katwa) 
  • Vitunguu swaumu punge 4 ( vimenywe na kupondwa pondwa) 
  • Karoti 2 ( kwangua maganda na kukata vipande vidogo vidogo) 
  • Majani machache ya Bay 
  • Chumvi kwa kiasi ambacho kwako wapenda 
  • Mafuta ya kupikia vijiko 2 vya mezani 
  • Mahanjumati Masala kijiko 1 cha mezani ( kama unayo - sio lazima) 
  • Siagi ya Butter vijiko 2 vya mezani ( sio lazima/optional) 
 JINSI YA KUPIKA

  1. Kwanza anza na kuikata kata nyama na kuichemsha hadi kuiva kabisa. Wakati wa kuchemsha nyama weka chumvi kidogo na majani ya Bay na iwe na maji ili kupata supu ya kutosha kutengeneza mtori wako. Kuchemka kwa nyama hadi kuiva mda utatengemea namna unayochemsha 
  2. Sasa nyama ikiwa inachemka ni mda wa kumenya ndizi na kuzikata kata vipande vidogo vidogo - uziweke kwenye maji. 
  3. Nyama ikiwa tayari; weka kando 
  4. Chukua chombo kingine ambacho sasa ndio kitatumika kupika mtori ivo kisiwe kidogo sana. Weka katika moto ongeza mafuta kisha weka kitunguu swaumu kikaange kidogo tu kisha weka vitunguu maji na karoti (na mahanjumati masala kama ipo) endelea kuvikaanga kwa muda kama daki 2-3 kisha weka ndizi koroga kidogo ili kuivisha ongeza ile supu ya nyama kidogo. Ivisha kwa dakika 10 - 15 hadi ndizi ziwe zimelainika ila supu ipungue. 
  5. Ukiona maji yamepungua na zimelainika sasa epua na anza kuziponda kama unasonga ugali hivi au unaponda kama ile wanaita mash potatoes. ukiwa wasonga na kama ile siagi ipo ndio mda wa kuweka. 
  6. Ukiona zimelainika vema anza kuongeza ile supu ya nyama kupata ulaini uupendao. 
  7. Baada ya kuupata ulaini mzuri wa mtori weka zile nyama kisha rudisha jikoni vichemke pamoja kwa dakia 3-5 . Baada ya hapo pishi la Mtori lipo tayari , pakua na kufurahia.

No comments:

Post a Comment

@chefkile