Jinsi ya Kupika Supu ya Maboga


Nikikumbuka juu ya maboga wakati wa utoto wangu ni kuwa nakumbuka zaidi tulikuwa tunachemshiwa asubuhi ndio inakuwa kitafunwa cha siku hiyo. Mbali na maboga kuwa matamu sana pia majani yake hutumika kama mboga katika familia nyingi sana hapa kwetu Tanzania na kwengineko. Ila leo nataka nikwambie namna ya kuandaa supu ya maboga ni supu nzuri na tamu sana pia ni rahisi sana kuandaa.

Supu kwa watu 3

MAHITAJI 


  • Boga 1/2 kg 
  • Karoti 3 ( zikatekate) 
  • Kitunguu maji 1 ( menya na katakata) 
  • Chumvi kwa kiasi upendacho 
  • Mafuta ya kula ( vegetable oil) kijiko kimoja cha mezani 
  • Maziwa freshi nusu lita (utayapasha moto kabla ya matumizi) 
  • Gharam Masala kijiko kimoja cha chai 
  • Pilipili kidogo - yaweza kuwa pilipili manga 1/2 kijiko cha cahi 

JINSI YA KUANDAA 



  1. Kwanza menya boga na kuondoa mbegu zote kisha ulikate kate vipande vidogo vidogo. Yaweke pembeni , Zile mbegu usitupe zichambue kisha osha na uzianike zinafaa kwa matumizi mengine. ( nimeelezea matumizi ya mbegu za maboga ukurasa wa ---) 
  2. Sasa andaa vitunguu na karoti. Vitunguu andaa kama kawaida ambavyo ungefanya kwa matumizi mengine, karoti zimenye na kuzikata kata. 
  3. Weka chombo katika moto na uweke mafuta ya kula pamoja na vitunguu, ivisha kidogo tu vitunguu kisha weka karoti, gharam masala, chumvi na pilipili kidogo kama ni mtumiji. Ivisha kidogo kisha weka maboga na maji kidogo wacha vichemke pamoja kwa kama daki 7 hadi 10 maji yawe yamepungua kidogo tu kama ikibidi uongeze maji basi ongeza maziwa. 
  4. Inapokuwa vimelainika vizuri na maji yamepungua basi weka kando na uanze kukanda kwa mwiko au kwa kutumia mashine ya kupondea ( blender), wakati wa kuponda ponda kama ikiwa na ugumu; ongeza maziwa ili kufikia kiwango cha ulaini ukipendacho. Baada ya hapo ni tayari kwa kula na waweza enjoy supu yako na kipande cha mkate.

No comments:

Post a Comment

@chefkile