Jinsi ya Kupika Viazi kwa Foil


Nilipata kugundua jinsi ya kuandaa viazi hivi vitamu kwa kula siku nikiwa nachoma nyama na mdogo wangu mmoja nyumbani kwangu. Na tulikuwa tukichoma katika yale majiko ya kufunika. Sasa baada ya kuweka nyama na ikiwa inaiva ndipo tukawaza kwanini na viazi tusiweke humo humo.

Hivyo tukachukua viazi na kuviosha vizuri; maana hatukutaka kumenya viazi; baada ya kuviosha ndipo tukaweka katika foil pamoja na viungo vingine na kuingiza kwenye jiko ambalo lilikuwa na joto la kutosha. Baada ya kupata matokeo mazuri nikaona ni vema niweke katika maandishi ili na wengine wajue namna ya kuandaa pishi hili zuri na rahisi sana kuliandaa.

Pishi vya kutosha watu 4 

MAHITAJI


  • Viazi 1kg 
  • Mafuta ya Kupikia kijiko kimoja cha mezani 
  • Chumvi kijiko kimoja cha chai 
  • Majani ya Bay moja au mawili 
  • Majani ya Rosemary vijani vya kujaa kijiko cha mezani 
  • Pilipili manga 1/2 kijiko cha chai 
  • Kitunguu swaumu punje 2 , menya na kuziponda ponda 

JINSI YA KUANDAA 



  1. Osha viazi vizuri kabisa 
  2. Andaa mchanganyiko wa viungo yaani; chumvi, pilipili manga, vitunguu swaumu na kwa hayo majani ni kuyaponda ponda . 
  3. Chukua foil ambayo itatoshea viazi vyako vyote, foil isiwe na maji maji; weka viazi na kisha changanya na hivyo viungo ongeza chumvi na mafuta ya kupikia. 
  4. Baada ya kuuweka vizuri mchanganyiko wa viungo sasa funga foil yako vizuri na uweke katika jiko ( inaweza kuwa jiko la kuoka [oven] au jiko la mkaa kawaida) . 
  5. Suala muda linategemea zaidi na kiasi cha joto lililopo - Ila kwa mda wa kuanzia dakika 30 viazi huwa tayari kwa kuliwa Sasa vikiwa vimeisha iva ni uamuzi wako tu ule na nyama choma kama sisi, ule na mtindi au na mboga yoyote kwa jinsi wapendelea. Furahia pishi - Asante

No comments:

Post a Comment

@chefkile